TFF YAMTANGAZA KIM POULSEN KUWA KOCHA MPYA STARS
Release No. 072
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 11, 2012
KIM KOCHA MPYA TAIFA STARS
Kim Poulsen ameteuliwa kuwa kocha mpya
wa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania (Taifa Stars) kuanzia Mei
11 mwaka huu kuziba nafasi ya Jan Poulsen.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam leo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema Kim amepewa mkataba
wa mwaka mmoja baada ya Shirikisho kuamua kutomuongezea mkataba Jan.
Mkataba wa Jan uliokuwa wa miaka miwili unamalizika Julai 30 mwaka huu.
Amesema kwa vile Taifa Stars inakabiliwa
na mechi za mchujo za Kombe la Dunia raundi ya pili Kanda ya Afrika na
mechi za mchujo za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN), TFF imeona ni
lazima iwe na kocha mpya mapema kabla ya mkataba wa Jan kumalizika.
Kim ambaye ni raia wa Denmark amekuwa
nchini kwa mwaka mmoja sasa akifundisha timu za Taifa za vijana wenye
umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) na miaka 20 (Ngorongoro Heroes),
hivyo anawafahamu vizuri wa wachezaji wa Tanzania.
TFF imeanza mchakato wa kutafuta kocha
mwingine wa timu za vijana atakayeziba nafasi ya Kim. Ili kuwa na
makocha wenye falsafa moja, kocha huyo anatafutwa kutoka Denmark.
Naye Kim ambaye Jumatatu (Mei 14 mwaka
huu) atatangaza kikosi cha Taifa Stars ambacho Juni 2 mwaka huu kuivaa
Ivory Coast katika mechi ya mashindano amesema yuko tayari kwa kazi hiyo
na kusisitiza kuwepo ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali ili timu
hiyo iweze kufanya vizuri.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MWANDISHI RACHEL MWILIGWA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mhariri wa Michezo wa gazeti la
Mtanzania, Rachel Mwiligwa kilichotokea leo (Mei 11 mwaka huu) katika
Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya
habari na mpira wa miguu kwani Rachel kwa kipindi chote akiwa mwandishi
na baadaye Mhariri alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango wake katika
mpira wa miguu tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu
Rachel, kampuni ya New Habari ambayo ndiyo inayomiliki gazeti za
Mtanzania na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Rachel mahali pema peponi. Amina
TWIGA STARS, ZIMBABWE KUUMANA LEO
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa
wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) na Zimbabwe zinapambana kesho (Mei 12
mwaka huu) katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayofanyika Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Twiga Stars ambayo ilikuwa katika ziara
ya mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma na Mwanza imerejea leo (Mei
11 mwaka huu) jijini Dar es Salaam tayari kuikabili Zimbabwe. Ikiwa
Mwanza jana ilicheza mechi ya kirafiki dhidi Rock City Queens, lakini
mechi hiyo ilivunjika dakika ya 58 kutokana na mvua kubwa. Hadi mechi
inavunjika, Twiga Stars ilikuwa ikiongoza kwa mabao 5-0.
Kwa mujibu wa kocha wa Twiga Stars,
Charles Boniface Mkwasa, mechi hiyo itakuwa kipimo kizuri kwao kabla ya
kucheza mechi ya mashindano ya Afrika (AWC) dhidi ya Ethiopia. Mechi
hiyo itachezwa Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa kabla ya kurudiana
Dar es Salaam wiki mbili baadaye.
Naye Kocha wa Zimbabwe, Rosemary Mugadza
amesema amefurahi kupata mechi hiyo kwa vile anaamini Twiga Stars ni
kipimo kizuri kwao kabla ya kucheza mechi yao ya AWC dhidi ya Nigeria.
Twiga Stars na Zimbabwe zilishakutana
mara mbili mwaka jana. Mara ya kwanza ilikuwa nusu fainali ya Kombe la
COSAFA ambapo katika mechi hiyo iliyochezwa Julai 5 jijini Harare,
Zimbabwe ilishinda kwa penalti 4-2.
Mechi ya pili ilikuwa michezo ya All
Africa Games (AAG) iliyofanyika Maputo, Msumbiji ambapo timu hizo
zilitoka sare ya mabao 2-2.
Viingilio katika mechi hiyo
itakayochezeshwa na mwamuzi wa kimataifa Judith Gamba kuanzia saa 10.30
jioni ni sh. 1,000 tu kwa sehemu zote isipokuwa VIP A ambayo ni sh.
10,000 na VIP B ambayo kiingilio chake ni sh. 5,000.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:
Post a Comment