OFFICIAL: LLOYD NCHUNGA ABWAGA MANYANGA YANGA
LLOYD NCHUNGA BIHARAGU
C/O LLOYD ADVOCATES,
Morogoro/Bibi TIti Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers
P.BOX 75111, Dar-Es- Salaam,Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA KLAB YA YANGA.
Ndugu
wana Habari, najua kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na
wanayanga wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao
vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita kwamba hakuna wa kujiuzulu kati
yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao tulipanga ufanyike tarehe
15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu linalotolewa na
baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa kamati ya
utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru
wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na
hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio
ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo.
Tangu
tumeingia madarakani tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu
katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa
ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati
(Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja kwa watani wetu wa
jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei
2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika
klab yetu.
Hali
kadhalika tumeshirikiana mpaka tumeweza kuboresha mkataba kati yetu na
TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia mkataba na kampuni ya
NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa wa mafia na uwanja wetu wa
KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati miliki za maeneo
yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za mwisho za
kumalizia michoro.
Hali
kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo
yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho yatokanayo na matakwa ya
sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa
inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na
kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na kukusanya
data za wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya
shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha
miaka mitatu. Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia
mapengo yaliyokuwa yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
Kwa
ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali
kwa ajili ya udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja katika hati ya
makabidhiano kwa kiongozi ajaye.
Aidha,
tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni
pamoja na sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka,
kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa, na kongamano la vijana
lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa ni
pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo maombi
yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.
Haya
yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana
muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo mtaona yalikuwa mazuri.
Lakini
pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja. Nichelee kusema tu kwamba
tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis
Mosha na mjumbe wetu ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo, kwani
tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala la kujiuzulu
ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili mkuu ambaye
sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali,
tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.
Ninachokiona
mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali
yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa
kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa mfululizo
wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonyesha kwamba
kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema.
Sioni
mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho
n.k. Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli,
ndiyo tuvune bao 5!
Kwa
wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali
mbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja
tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili,
sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali.
Hata
hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo
itatula kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka
wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia.
Baada
ya mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee
kupitia msemaji wao , Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha
Michezo cha Redio moja maarufu hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga
ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza!
Hii
imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake
wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu.
Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko
kumkata nusu.
Kwa
hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga
kwani ni klab ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya
28 ya katiba yetu.
Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi.
Natumaini
kamati ya utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya
29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza
wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa mafanikio zaidi.
Nitaendelea
kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale
nitakapo hitajika na nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.
Wasalaam,
LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.
Nakala kwa:-
Mama Fatma Karume,Mdhamini
Francis Kifukwe, Mdhamini
Bwana Yusuf Manji – Kwa taarifa
Kwa hisani ya Shaffih Dauda

No comments:
Post a Comment