CHADEMA yafunika Dar
LICHA
ya Jeshi la Polisi kutoa amri wananchi na wakazi wa Mkoa wa Dar es
Salaam wasiandamane kuelekea katika viwanja vya Jangwani jana kuhudhuria
mkutano wa hadha ra wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
viwanja hivyo vilifurika umati wa wananchi kwa kiasi kikubwa huku
utulivu ukitawala.
Umati
huo ulianza kuingia uwanjani hapo majra ya asubuhi huku kukiwa na
vibanda 16 vilivyokuwa vikisimamiwa na vijana kutoka vyuo vikuu ambao ni
wanachama wa CHADEMA kwa ajili ya watu kujiunga na chama hicho na
wengine kurudisha kadi za vyama vingine.
Kutokana
na zoezi hilo la kurudisha kadi na kupata wanachama wapya, jumla ya
watu 3,124 walijiunga na CHADEMA jana katika viwanja hivyo akiwamo mzee
Raphael Koimere, aliyekuwa kada maarufu wa CCM.
Majira
ya saa 9:20 mchana msafara wa wapanda pikipiki zaidi ya 200 uliwasili
uwanjani hapo huku wengine wakiwa na mabango ya kuhamasisha na kuelezea
kasoro za kufanyiwa kazi.
Miongoni
mwa mabango hayo yaliyosema: ‘Jimbo la Ilala linawaangusha Watanzania
katika mageuzi ya kweli kwa kuwa mipango yote ya ufisadi huanzia hapo na
kutekelezwa katika ofisi zilizo katika wilaya hiyo’.
Mabango
mengine yalisomeka: ‘Shibuda ulikuja CHADEMA kwa mkopo na sasa
hatukutaki, rudi ulikotoka’, ‘Tunamuomba CAG akague hesabu katika ofisi
za mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala na jingine likiwatahadharisha CCM
muda wao wa kuwa madarakani umekwisha waanze mazoezi ya kuwa wapinzani
wa kudumu, kama si kupotea katika ramani ya kisiasa ya Tanzania.
Majira
ya saa 9:30 mchana viongozi mbalimbali wa CHADEMA walianza kuwasili
uwanjani hapo wakiwamo wabunge wa chama hicho wakiongozwa na John
Mnyika, Mbunge wa Ubungo.
Baadhi
ya viongozi waliowasili uwanjani hapo ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbles Lema, wanasheria maarufu nchini Mabere Marando,
Profesa Abdallah Safari na Edson Mbogoro, huku wanachama waliojiunga na
CHADEMA hivi karibuni kutoka mkoani Arusha James ole Milya na Ally
Bananga wakiwa ni miongoni mwa watu waliokaa meza kuu.
Ilipofika
saa 9:54 Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA aliwasili uwanjani hapo huku
akifuatiwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, hali iliyoamsha
shangwe kubwa kutoka kwa wananchi waliokusanyika uwanjani hapo.
Baada
ya kuketi viongozi hao, mkutano ulifunguliwa kwa dua kutoka kwa
viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo na kisha baadhi ya viongozi
wakaanza kuzungmza huku viongozi watatu wakiwa ndio wasemaji wakuu
katika mkutano huo, ambao ni Freeman Mbowe, Dk. Willibrod Slaa na Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lisu.
Mbowe akemea udini, ukabila
Akizungumza
katika mkutano huo Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe,
akihimiza kuwekwa mbele kwa masilahi ya taifa badala ya vikundi vya watu
wachache.
Alisema
ni wakati wa Watanzania kutambua haki zao na kuwaonya viongozi wa
serikali ili kuacha mtindo wa kuligawa taifa kwa dhana ya udini, ukabila
na ukanda.
“Ninaliongea
hili kwa kuwa kuna watu sasa hawajui hatima yao na wamebaki katika
kukumbatia suala zima la udini, ukanda na ukabila kuligawa taifa, mimi
ninawaambia Watanzania, sisi CHADEMA kama chama kinachojipanga kuchukua
dola tunamhitaji kila mmoja mwenye sifa ya Utanzania, pasipo kujua dini
yake, kabila lake, wala anatoka ni eneo gani la nchi,” alisema Mbowe.
Akizungumzia
utata wa kauli mbalimbali za baadhi ya wanachama ndani ya CHADEMA,
Mbowe alisema hawataweza kumvumilia mtu yeyote mwenye dhamira ya
kuvuruga umoja ndani ya chama hicho kwa masilahi yake na kundi lake.
Akizungumza
kwa hisia kali, pasipo kutaja jina la mtu, licha ya maongezi hayo
kuonekana yakimlenga Mbunge John Shibuda, Mbowe alisema: “Hatua ya
kuifikisha CHADEMA hapo ilipo ilianza miaka 20 iliyopita na kwamba
akitokea mtu wa kuivuruga, taratibu za kumuwajibisha zitafuatwa.
“Kauli
ya chama ni makini, hakitayumbishwa na propaganda za mapandikizi na
hata wasio na nia nzuri na nchi. Tutafanya maamuzi mazuri kwa njia ya
haki na tusimfikirie mpuuzi mmoja kutuharibu, yeyote atakayechezea moto
utamchoma,” alisema Mbowe.
Akilizungumzia
Jeshi la Polisi na hali ya amani, Mbowe alisema jeshi hilo liache
kutumika kwa masilahi ya CCM na badala yake lifanye kazi kwa maadili ya
jeshi hilo.
Alisema
licha ya uchokozi unaofanywa mara kwa mara na viongozi wa CCM kwa
kulitumia Jeshi la Polisi kuvuruga amani ya nchi, chama hicho kitakuwa
cha mwisho kuelekea katika uvunjifu huo wa amani.
“Ndugu
zangu Polisi watambue njia ya kuelekea amani ya kudumu ni kuheshimu
demokrasia, wasitumie ofisi zao kunyanyasa, kuwatesa na kuwapiga
wananchi, hali hii ikome kuanzia sasa,” alisema Mbowe.
Akitumia
nukuu ya Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela,
Mbowe alisema serikali yoyote inayotumia nguvu na majeshi kwa ajili ya
kuulinda utawala wa kidhalimu, ndiyo inayowafundisha raia wa nchi hiyo
kutumia nguvu kuwapinga.
Alisema
harakati za mabadiliko yanayofanywa sasa na chama hicho kupitia
kaulimbiu yao ya (M4C) ni maandalizi ya kushika dola mwaka 2015 na
kuwataka wananchi kushiriki kwa kila namna katika harakati hizo.
Dk. Slaa atoa mikoba
Katibu
Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alisema taifa lipo katika hali
ngumu ikiwamo, mfumuko wa bei, unaosababisha kupanda kwa gharama za
maisha kunakochangiwa na na matumizi mabaya ya serikali.
Alisema
jambo jingine linalochangia hali ngumu ya maisha ni pamoja na rais kuwa
na mamlaka makubwa ya uteuzi pasipo kushauriana na mtu, hali
inayomfanya aonekane kama mungu mtu.
“Serikali
ina matumizi makubwa kiasi cha kupelekea taifa katika umasikini na
hakuna mwananchi wala wabunge kuhoji na akapatiwa jibu, kwani ukihoji
unaambiwa mamlaka ya rais hayahojiwi, si wewe na mimi wala wabunge na
mawaziri wake,” alisema Dk. Slaa.
Akielezea
zaidi, Dk. Slaa alisema, rais amekuwa akigawa vyeo kwa kutumia mamlaka
yake vibaya katika nafasi mbalimbali ikiwamo kwa waliompa hifadhi,
marafiki, ndugu na wale waliomsaidia kuingia Ikulu huku akihoji ukubwa
wa baraza la mawaziri.
Alitolea
mfano Uingereza kuwa waziri mkuu, ana mamlaka ya kuchagua mawaziri 20
tu, na akizidisha zaidi ya hapo atalazimika kumlipa kwa hela yake ya
mfukoni na si kodi za wananchi.
Aidha,
aliwataka wabunge wa chama hicho kutetea masilahi ya wananchi
watakapoingia katika Bunge la bajeti litakaloanza Juni 12 na kwamba kama
watazomewa na watu wasitake wananchi watetewe, litakuwa ni jukumu la
wananchi kuwazomea wakirudi katika majimbo yao.
Lissu
Ilipofika
zamu ya Tundu Lissu kuzungumza, wananchi walimlazimisha avue kofia yake
aina ya ‘Pama’ ili waweze kumuona na alipofanya hivyo wakalipuka kwa
shangwe kwa kuimba ‘jembe, jembe, jembe’ hadi Mbunge wa Mbeya Mjini,
Joseph Mbilinyi (Sugu) aliposimama na kuwaomba watulie.
Akihutubia
mkutano huo, Lissu alijikita katika suala zima la wananchi kufahamu
umuhimu wa Katiba na kuweza kutoa maoni yatakayohitimisha utawala wa
kichifu nchini.
Alisema
licha ya suala hilo kupigiwa kelele na watu mbalimbali serikali ya CCM
imekubali mchakato huo kwa hila huku ikitunga sheria hovyo ya kuupeleka
bungeni, wakitumia wabunge waliopo kwa kuamini wapo wengi na hivyo
watapitisha kwa masilahi yao na chama chao.
Aliongeza
kuwa hata hatua ya kuzuia masuala ya muungano yasijadiliwe ni njia moja
wapo ya matumizi mabaya ya madaraka, kwa kuwa suala hilo haliwezi
kutenganishwa na Watanzania.
Aliwataka
wananchi kuhakikisha tume ya maoni ya Katiba itakapowafikia wawe na
ujasiri wa kuuliza nafasi ya Tanganyika katika Serikali ya Muungano kwa
kile alichosema mpaka sasa baada ya Zanzibar kurekebisha katiba yao
Tanzania haijulikani ina nchi ngapi, wakuu wa nchi wangapi na maamiri
jeshi wangapi.
Alisisitiza
Watanzania wasisite kutaka kuwepo kura ya maoni kuangalia kama
yaliyofanyika Zanzibar ni sawa kwa ustawi mzima wa muungano.
Aidha,
Lissu alisema kwa utaratibu wa sasa bunge litakapokaa kama bunge la
katiba ni wazi CCM na washirika wake watakuwa zaidi ya 400 na kutaka
suala hilo lihusishe watu wa kada mbali mbali pasipo kujali vyama vyao
kwa ajili ya kupig kura hiyo katika bunge la katiba.
Akizungumzia
mamlaka ya uteuzi, Lissu alisema yanatumika vibaya kwa kuwa katika
Bunge tayari kuna theluthi moja ya wabunge ambao kazi yao ni kugonga
meza kwa ajili ya kupongeza kila kitu kwa kuwa hawawajibiki kwa wanchi.
Lema
Aliyekuwa
mbunge wa Arusha Mjini Godbles Lema, akizungumza katika mkutano huo
alisema yupo kwenye ‘honeymoon’ na kwamba wakati wowote atarudi kazini
kuwatumikia wananchi wa Arusha.
Alisema
kwa hali ilivyo sasa siyo lazima kufika mwaka 2015 kama viongozi wa
serikali wataendelea kufanya ubadhirifu unaosikika kila kunapokucha.
Alibainisha
hali hiyo ya ubadhirifu ndiyo inayosababisha kuwepo na machangudoa,
majambazi na hata omba omba licha ya kuwa ni nchi tajiri na inayoshika
nafasi ya tatu kwa kuwa na almasi zilizo bora kidunia.
Naye
Mbunge wa Ilemela, Ezekia Wenje, alisema nchi ya Tanzania ni kubwa
kuliko Mtanzania yeyote aliyeko CHADEMA, CCM na hata vyama vingine na
kwamba kila mmoja ana wajibu wa kutunza amani.
Kwa
upande wake, Halima Mdee, alisema umati wa watu uliojitokeza katika
mkutano huo unaashiria kuwa Dar es Salaam, hakukaliki kwa upande wa CCM,
na kuondoa dhana waliyokuwa wakijivunia CCM kuwa Dar ni ngome yao.
CHANZO - Tanzania Daima
Kwa hisani ya chademablog.


No comments:
Post a Comment