TFF YAIPA AZAM POINT 3 NA MAGOLI 3-0 DHIDI YA MTIBWA SUGAR
Release No. 064
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 26, 2012
MECHI YA TWIGA STARS, ZIMBABWE YAFUTWA
Mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya
timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) na Zimbabwe iliyokuwa ichezwe
keshokutwa (Aprili 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
imefutwa.
Uamuzi huo umefanywa na Chama cha Mpira
wa Miguu Zimbabwe (ZIFA) ambayo sasa imeamua kucheza mechi ya kirafiki
na Zambia. Mechi hiyo itachezwa Aprili 28 mwaka huu jijini Harare.
Twiga Stars inaendelea na mazoezi chini
ya kocha wake Charles Boniface Mkwasa katika kambi ya Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT) iliyoko Ruvu mkoani Pwani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linaendelea na jitihada za kuitafutia mechi za kirafiki Twiga
Stars kabla ya kucheza mechi ya mashindano dhidi ya Ethiopia ambayo
itafanyika Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa.
MTIBWA SUGAR YAPOTEZA MECHI DHIDI YA AZAM
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) imemuondoa mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma kwenye
orodha ya waamuzi kwa kuvuruga mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Azam
na Mtibwa Sugar iliyochezwa Aprili 23 mwaka huu.
Pia waliokuwa waamuzi wasaidizi wa mechi
hiyo; Samuel Mpenzu na Abdallah Uhako wote kutoka Arusha nao
wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Vilevile Kamati imeipa Azam ushindi wa
mabao 3-0 kwa mujibu wa Ibara ya 31 ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Kwa mujibu wa kanuni hiyo, timu
itakayohesabika kupoteza mechi (Mtibwa Sugar) itakuwa imefungwa mabao
3-0.
Kwa mujibu wa Kanuni ya Ligi Kuu ya
Vodacom kifungu cha 22(3-6) Mtibwa Sugar imepigwa faini ya sh. 500,000,
imepoteza mapato yote ya mchezo huo na inatakiwa kulipa faini hiyo kabla
ya mechi inayofuata.
Nao makamishna watatu; Abdallah Mitole
wa Dar es Salaam, William Chibura (Musoma) na Omari Mawela (Mwanza)
wameondolewa kwenye orodha ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kushindwa kufika
kwenye mechi walizopangiwa kusimamia bila taarifa.
Makamishna hao wametakiwa kutoa maelezo
ya maandishi wakieleza sababu za kutofika kwenye mechi. Mechi walizokuwa
wamepangia ni Coastal Union vs Ruvu Shooting (Mitole), Kagera Sugar vs
Yanga (Chibura) na Kagera Sugar vs African Lyon (Mawela).
Nayo Moro United imepigwa faini ya sh.
500,000 baada ya wachezaji wake kugoma kuingia kwenye vyumba vya
kubadirishia (dressing rooms) wakati wa mechi namba 171 kati yao na
Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa kanuni ya 8(16).
Pingamizi la Villa Squad dhidi ya
African Lyon kuwa wakati wa mechi yao ilitumia wachezaji wawili (Mohamed
Samata na Benedict Jacob) ambao mikataba yao imemalizika limetupwa kwa
vile wana leseni halali za kucheza ligi.
Pia mwamuzi wa mechi namba 160 kati ya
Moro United na Oljoro JKT, Nathaniel Lazaro wa Kilimanjaro amefungiwa
miezi sita na kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa kutozingatia
kutunza muda kwa mujibu wa kanuni ya 26(1)(f).
Vilevile Kamishna wa mechi ya Moro
United na Oljoro JKT, Ali Mkomwa wa Pwani na Said Mnonga wa Mtwara
aliyekuwa mwamuzi msaidizi mechi kati ya Villa Squad na Coastal Union
wameandikiwa barua za onyo wakitakiwa kuwa makini kwenye michezo
wanayosimamia.
9 POLISI WAPIGWA FAINI MIL 1/- KILA MMOJA
Kamati ya Ligi ya TFF imewafungia mechi
tatu na kuwapiga faini y ash. milioni mmoja kila mmoja wachezaji tisa wa
timu ya Polisi Dodoma baada ya kumpiga mwamuzi Martin Saanya kwenye
mechi dhidi ya Azam iliyochezwa Aprili 14 mwaka huu mjini Dodoma.
Wachezaji hao walioadhibiwa kwa mujibu
wa kanuni ya 25(g)(iii) ni Noel Msekwa, Frank Sindato, Abdallah Matila,
Bantu Admin, Salmin Kisi, Madope Mwingira, Sihaba Mkude, Kaliyasa
Mashaka na Ibrahim Massawe.
Iwapo wachezaji hao watahama Polisi na kujiunga na timu nyingine, watahama na adhabu zao.
Vilevile timu ya Polisi Dodoma imepigwa
faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake katika mechi
hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri. Pia timu hiyo imepewa barua ya onyo
kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi yao na Yanga
iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)


No comments:
Post a Comment